Dodoma, Ijumaa, Juni 6, 2025

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST), Prof. Carolyne Nombo leo (Ijumaa, Juni 6, 2025) amezindua miongozo ya utoaji mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa elimu ya juu na vyuo vya kati kwa mwaka 2025/2026 kuanzia ngazi ya Stashahada hadi Shahada za Juu.

Katika hotuba yake iliyoandamana na uzinduzi rasmi wa miongozo hiyo, Profesa Nombo amesema miongozo hiyo itachapishwa katika tovuti za HESLB na WyEST ili kuwapa fursa waombaji mikopo na wadau wengine kusoma miongozo hiyo kabla ya dirisha la uombaji mikopo kufunguliwa.

Miongozo itaanza kupatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Elimu (www.moe.go.tz) na tovuti ya Bodi ya Mikopo (www.heslb.go.tz). Ninawashauri wanafunzi, wazazi na walezi waisome na kuzingatia maelekezo yaliyomo”, amesema Prof. Carolyne Nombo.

Hafla ya uzinduzi imefanyika katika ukumbi wa Seneti wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambapo wadau mbalimbali akiwemo Makamu Mkuu wa Chuo cha UDOM Prof. Lughano Kusiluka ameshiriki na kusema chuo hicho ni miongoni mwa vyuo ambavyo wanafunzi wake wananufaika na mikopo na ruzuku zinazotolewa na serikali kupitia HESLB.

Wadau wengine walioshiriki katika hafla hiyo walikuwa viongozi wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu na Kati (TAHLISO na ZAHILFE), Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Awali, akitoa neno la utangulizi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Bw. Elihuruma Lema amesema kuwa HESLB imejiandaa na iko tayari kupokea maombi ya mikopo ya wanafunzi kuanzia Juni 15, 2025 hadi Agosti 31, 2025.

See also  HESLB: Sifa Za Kupata Mkopo wa Bodi Ya Mikopo Tanzania

“Kuanzia Juni 15, 2025, mwombaji atapaswa kuingia kwenye tovuti ya HESLB www.heslb.go.tz kisha atabofya kiunganishi ‘Loan Application’ kwa kutumia Namba ya Kidato cha Nne na kufuata maelekezo. Mwisho wa kupokea maombi ya mikopo utakuwa Agosti 31, 2025 amesisitiza Mkurugenzi Lema.

Miongozo ya utoaji mikopo na ruzuku kwa wanafunzi iliyozinduliwa leo ni maandalizi ya kupokea maombi na hatimaye kupanga mikopo kwa wanafunzi wahitaji wenye sifa. Miongozo hiyo ni ya Stashahada (Diploma), Shahada za awali (Bachelor Degree), Stashahada ya Juu ya Sheria kwa Vitendo (Law School), Shahada za Uzamili na Uzamivu, na  Ruzuku (Samia Scholarship).

Katika kipindi cha miaka minne iliyopita (2020-2021 hadi 2024-2025), Serikali imeongeza bajeti ya fedha za mikopo ya elimu kutoka TZS 464 bilioni (2020-2021) hadi TZS 787 bilioni mwaka unaomalizika wa 2024/2025. Katika mwaka mpya wa masomo 2025/2026 utakaoanza mwezi Oktoba, 2025, bajeti iliyoidhinishwa ni TZS 916.7 bilioni inayotarajiwa wanafunzi 252,773.

Categorized in:

Tagged in: